USHAWISHI mkubwa umefanywa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuhakikisha kuwa, katibu mkuu aliye mapumzikoni wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Wallboard Slaa anashiriki kwenye kampeni ya chama hicho tawala, Uwazi Mizengwe limeambiwa. Chanzo kutoka ndani ya CCM kilisema hivi karibuni kuwa, mazungumzo yamefanikiwa kwa kiwango kikubwa na kwamba upo uwezekano wa asilimia 90 kwa Dk. Slaa kupanda jukwaani siku ya ufunguzi wa kampeni za CCM uliopangwa kufanyika kwenye Viwanja vya Jangwani, Dar keshokutwa Jumapili. “Ili kukabili nguvu ya upinzani tulipanga kuwa Dokta atoke mafichoni ashiriki nasi kwenye uzinduzi, tuna imani hilo litafanikiwa na utakuwa ni mtaji mkubwa kwa chama chetu kipindi hiki cha kuelekea kwenye uchaguzi mkuu,” kilisema chanzo chetu.
DK. SLAA AMEKUBALI?
Kwa mujibu wa chanzo hicho, pamoja na kutamka wazi kuwa mazungumzo yamefanikiwa kwa kiwango kikubwa lakini suala la ushiriki wa kiongozi huyo kutoka chama cha upinzani kwenye uzinduzi wa kampeni za chama tawala lilikuwa halijaafikiwa na Dk. Slaa kwa asilimia mia moja. “Bado kuna mambo madogomadogo yanakwamisha lakini wakubwa (chanzo hakitaji kwa majina wakubwa ni akina nani lakini kwa tafsiri huenda ni viongozi wa CCM ngazi ya taifa) wamepanga kukutana naye na kufikia makubaliano.” Aidha, Mwandishi Wetu alipodadisi mambo hayo madogomadogo ni yepi, chanzo hicho hakikuweka wazi lakini uwepo wa maafikiano ya hatima ya
kisiasa ya Dk. Slaa lilikuwa jambo la wazi.
KWA NINI DK. SLAA AIPIGIE KAMPENI CCM?
Chanzo ndani ya CCM ambacho kimo kwenye timu ya ushindi ya chama hicho iliyotangazwa hivi karibuni kilisema: “Hakuna kitu kingine zaidi ya kummaliza mpinzani wetu (Edward Lowassa ambaye ni mgombea kutoka vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi kwa kufupi Ukawa.) “Kwenye uzinduzi tumepanga dokta apande jukwaa moja na mgombea wetu (John Pombe Magufuli)wafanye mashambulizi, tumalize kazi na tusubiri kuapishwa. Unadhani wapinzani watakuwa na nguvu tena baada ya hapo? Hakuna,” chanzo kilimaliza kwa kicheko. Mazungumzo kati ya mwanasiasa huyo machachari na CCM si habari mpya kwani imekwisharipotiwa mara kadhaa na vyombo mbalimbali vya habarri bila kukanushwa na Dk. Slaa ambaye toka amejiondoa ndani ya Chadema amekuwa hataki kuzungumzia waziwazi hatima yake kisiasa.
UKAWA HOFU TUPU
Tangu Dk. Slaa ajiondoe Chadema, mwanasiasa huyo amezua hofu miongoni mwa wafuasi wa Ukawa kwamba kutokuwepo kwake kwenye umoja huo kunaweza kupunguza kura za upinzani na kuifanya CCM ipate ushindi mwingine wa tano baada ya mfumo wa vyama vingi na hivyo kuendelea kushika dola. “Hapo ni chumba cha habari cha Global? Nasikia Dk. Slaa kajiunga CCM?” alihoji mdau wetu wa habari na mfuasi wa Chadema kutoka Karatu mkoani Arusha aliyejitambulisha kwa jina moja la Jofrey ambaye alitaka kupata uthibitisho juu ya uvumi wa mwanasiasa huyo kuhamia chama tawala.
Hata baada ya kuambiwa kuwa habari hizo hazina uthibitisho wa moja kwa moja, shabiki huyo wa Ukawa aliongeza: “Laa! Sawa kaka kama unanificha sawa, ila huku hatuna raha kabisa. Yule mzee akijiunga CCM, itakuwa shida sana Ukawa kupata ushindi.” MAJIBU YA CCM Kwa upande wa CCM, msemaji wake ambaye pia ni Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye alipotafutwa na mwanadhisi wetu hakuweza kupatikana lakini mmoja kati ya viongozi waandamizi wa chama hicho ambaye hakupenda kutaja jina lake kwa sababu yeye si msemaji alikuwa na hayaa: “Sina taarifa za Dk. Slaa kujiunga na chama chetu wala sijui kama atatambulishwa kwenye uzinduzi wa kampeni zetu, lakini kwa sisi ambao tulikwenda vitani tunasema Silaha ya vita haitupwi.” Hakufafanua kama Dk. Slaa ndiye silaha ya vita au la!
DK. SLAA ANATAFUTWA
Baada ya uwepo wa habari hiyo, jana gazeti hili lilimtafuta Dk. Slaa lakini kama mazoea ya siku za hivi karibuni kiongozi huyo wa zamani wa Chadema hakuweza kupatika kwa njia ya simu na hata alipofuatwa nyumbani kwake, Mbweni jijini Dar haikuwezekana kukutana naye ili azungumzie madai ya kukikampenia CCM. Hata hivyo, mmoja kati ya watu wake wa karibu ambaye hakupenda kutajwa jina lake alikana katakata taarifa hiyo kwa madai kuwa, hizo ni siasa za kujipatia ushindi kupitia nguvu za mtu mwingine. “Hivi unadhani dokta ni mtu mwepesi kiasi hicho? Huyu ni mtu wa misimamano sana. Sema watu wamekuwa wakitumia jina lake kujiongezea nguvu za kisiasa. Hawezi kupanda jukwaani kuinadi CCM, niamini mimi,” alisema.
UWAZI LACHUNGUZA ZAIDI
Kufuatia taarifa ya Dk. Slaa kuibukia kwenye kampeni kuzagaa na kudokezwa na gazeti moja la kila wiki hapa nchini, timu ya Uwazi Mizengwe iliingia katika uchunguzi kwa lengo la kuchimba zaidi ukweli wa mambo. Katika uchunguzi wake, timu hiyo ilibaini kuwepo kwa mazungumzo kati ya mwanasiasa huyo na CCM na kwamba kinara wa ushawihi huo ni kada maarufu wa chama ambaye amepata kuwa kiongozi mkuu kwenye nchi hii. Uwazi liliambiwa na chanzo kingine kuwa, Dk. Slaa alikwisha kuafikiana na mapendekezo ya CCM tangu mwishoni mwa mwezi uliopita na kwamba alikuwa akimsubiri mwenyekiti wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete arejee kutoka ziarani (nchini Australia) ili kumalizia ngwe ya mwisho ya makubaliano. Hata hivyo, mpaka tunakwenda mitamboni ilikuwa haijafahamika kuwa baada ya rais kurejea kutoka ziarani alikutanishwa na mwasiasa huyo na kumalizia mazungumzo au jambo hilo halijafanyika na kuvifanya vikwazo vidogovidogo vilivyotajwa na chanzo chetu cha awali kutoondolewa.
HALI ILIVYO MITAANI
Uchunguzi unaonesha kuwa hali ya kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu ni 50 kwa 50 na kwamba hakuna chama chochote chenye uhakika wa asilimia mia moja wa kuibuka na ushindi wa kiti cha urais. Baadhi ya wachunguzi wa mambo ya kisiasa wanasema CCM ina nafasi kubwa ya kupata ushindi lakini si wa kishindo huku wengine wakitabiri uwezekano wa Ukawa kupata ushindi wa kushtukiza utakaotokana na migawanyiko ya wanasiasa na makada wa chama hicho tawala inayokitikisa chama mwaka huu.
CHANZO: UWAZI MIZENGWE YA UCHAGUZI - Global Publishers
No comments:
Post a Comment