Monday, August 17, 2015

JULIUS MTATIRO: CCM INAWATUMIA WAJUMBE WA TUME YA WARIOBA KUJISAFISHA

Siasa imechukua nafasi kubwa sana nchini, zikitengeneza ‘story’ kila kukicha kuelekea uchaguzi mkuu Oktoba mwaka huu.

Aliyekuwa naibu katibu mkuu wa CUF Tanzania bara na mtangaza nia wa jimbo la Segerea Julius Mtatiro, amedai wajumbe wa tume ya kukusanya maoni ya katiba mpya iliyoongozwa na Jaji Warioba, wanatumika kukisafisha Chama Cha Mapinduzi CCM na kuudhoofisha Umoja Wa Katiba ya Wananchi UKAWA.

Mtatiro alitumia ‘time’ yake kupembenua mdahalo uliofanyika jana Jumapili Chuo kikuu Dar es salaam, ulioandaliwa na Taasisi ya Mwalimu Nyerere.

Tazama waraka wake hapo chini ‘then’ tuachie maoni yako.

“Leo nimeshangazwa sana kuwaona wazee naowaheshimu sana kama Butiku wakiishambulia UKAWA na maamuzi yake ya kumchukua Edward Lowassa kuwa mgombea urais wake. Butiku anasema anamfahamu vizuri Lowassa (nadhani kwa machafu ya Lowassa), amemshutumu kuhusu kuanzisha mtandao ndani ya CCM na kukivuruga chama hicho. Nakubaliana naye kwa kiasi fulani lakini nina maswali machache ya kumuuliza.

Mosi, mtandao ambao leo Butiku anauona hatari kwa mara ya kwanza ulikuwa mkakati wa moja kwa moja uliobuniwa na Kikwete na Lowassa na ndio uliomuingiza madarakani Kikwete (ambaye Butiku amemsifia) – Hapa tunarudi kwenye dhana ileile ya Nguruwe sili nyama yake ila nakunywa mchuzi wake. Kama Mzee Butiku na wenzake wanaamini Mtandao ulikuwa kundi hatari sana lakini wakaliacha likakua hadi likamuingiza madarakani Kikwete likifanya hivyo ndani ya CCM, leo wanaona dhambi gani Lowassa akitumia mtandao kuingia madarakani akiwa UKAWA. Mbona wakati mtandao una nguvu kubwa zaidi iliyomleta Kikwete madarakani Mzee Butiku na wenzake hawakung’aka? Walikaa kimya hadi Kikwete akaingia madarakani na kuunda serikali dhaifu sana ambayo imeliporomosha taifa zaidi katika kila sekta (kimaadili, kiuchumi, kimaendeleo, kiufisadi n.k.)

Pili, ni majuzi tu tulipokuwa kwenye Bunge Maalum la Katiba yeye Mzee Butiku na wazee wenzake wanaoheshimika sana walikuja na rasimu bora ya katiba ya watanzania ikiwa na lengo la kusaidia kuhuisha mfumo na kuisaidia serikali kubadilika. CCM ikiongozwa na Mwenyekiti wake wa chama (JK) iliipinga rasimu ile hadharani na kukataa karibia kila jambo jema lililomo. Naamini rasimu ile ilikuwa na malengo mapana ikiwemo (huwenda) kuvidhibiti vyama visijiundie wana mtandao watakaosaka madaraka, kitendo cha JK na CCM kuitupa mbali rasimu ile na kujitungia rasimu ya CHENGE na SITTA ambayo haina meno ya kudhibiti wanamtandao kama kina Lowassa (ikiwa tu mitandao ni jambo hatari sana), leo hii mzee Butiku anawezaje kuanza kuipigia debe CCM ambayo imekataa kabisa kujihuisha kimfumo, imeikataa katiba yenye maadili na kwa hiyo imekataa kabisa hatua za kikatiba ambazo zingeweza kuwadhibiti hao anaowaita wanamtandao ili wasiidhuru nchi kupitia chama chochote kile?

Tatu, ilikuwaje kuwaje yeye na Wenzake wanajua mambo machafu ya viongozi kama Lowassa na kuyakalia kimya, ilikuwaje akaendelea kuwa kiongozi ndani ya CCM, ilikuwaje akaendelea kupitishwa kuwa mbunge wa chama hicho kila mara, ilikuwaje akateuliwa na CCM kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ulinzi na Usalama wa Nchi, ilikuwaje akateuliwa na CCM na mwenyekiti wa CCM kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hadi alipoamua kujiuzuru mwenyewe? (maana alikuwa na uhuru wa kukataa kujiuzulu kama alivyofanya Pinda kwenye ESCROW), imekuwaje CCM inakaa na watu wachafu inawafanya kuwa wabunge, inawafanya kuwa mawaziri na inawafanya kuwa mawaziri wakuu na siku wakihama chama hicho inasema ni wachafu sana? Je, ndiyo kusema kwamba CCM ni chama cha kufuga wezi, wana mitandao, wavuruga vyama na watu wenye nia mbaya sana na nchi hii? Na kama ndivyo kwa nini bado Butiku anataka watanzania waendelee kuichagua CCM yenye sifa hizo?

Nne, Mzee Butiku alitiwa hofu sana na kitendo cha wajumbe wa NEC wa CCM kusimama na kuimba “wana imani na Lowassa!” na anasema kuwa kitendo kile ni kama mapinduzi kwa Kikwete ama kumdhalilisha sana na kwamba Kikwete alikuwa na OPTION ya kumkamata Lowassa na kumuweka ndani. Mzee Butiku atafakari pamoja na sisi kwamba ilikuwaje mwanachama mmoja anakuwa na nguvu kiasi hicho ndani ya CCM na akaachwa awe na nguvu hizo halafu analalamikiwa kwa kuwa na nguvu baadaye? Kama CCM ilimuona ni mchafu sana kwa nini ilimruhusu hata kuchukua fomu wakati inajua kuwa ni mtu hatari sana. Na yeye Butiku anadhani ni rahisi tu kwa kiongozi wa nchi kumuweka ndani kiongozi mwenzake kwa sababu ya kutofautiana kidemokrasia?

Tano, ikiwa Jakaya Kikwete aliingia madarakani kwa kutumia MTANDAO na kwamba mtandao huo ni hatari sana, maana yake ni kwamba Kikwete aliingia madarakani kwa njia za “Kihuni”, kama Butiku ni mtu wa maadili na analisimamia Taifa kwa nini mara kadhaa amekubali uteuzi aliopewa na Rais Kikwete ili kufanya kazi mbalimbali za nchi ili hali anajua kuwa huyu ni kiongozi aliyeingizwa madarakani kwa njia ya mitandao? Na ikiwa Butiku ameweza kumvumilia Kikwete kwa miaka 10 akiwa kimya huku akijua aliingia madarakani kwa mitandao hatari ndani ya CCM, anashindwa nini kuvumilia miaka mingine 10 kwa Lowassa kuingia Ikulu kwa kutumia mitandao lakini akitokea kwenye vyama vya upinzani?

Na mwisho, Mzee Butiku na wenzake watueleze, mbona chama wanachokitetea majuzi kwenye uchaguzi wa ndani ya chama wagombea wake karibia wote nchi nzima walikuwa wakigawa pesa kama karanga huku na kule tena bila hofu? Mzee huyu haoni kuwa SULUHISHO la pekee lililobakia mikononi mwa wananchi ni KUIONDOA CCM kwanza ili ikapumzike halafu kama bado inapendwa sana itakuja kurudi siku za usoni. Na ama mzee Butiku anataka kutueleza kuwa ni BORA TU WANZANIA WAENDELEE KUCHAGUA CCM ile ile yenye mamia na maelfu ya watuhumiwa wa ufisadi akiwemo mgombea urais wake au waamue kuchagua UKAWA yenye mtuhumiwa mmoja wa UFISADI huku ikija na taratibu mpya za uongozaji wa nchi?”

CHANZO: TIMES FM

No comments:

Post a Comment