Friday, September 4, 2015

Barua Kwa James Mbatia kutoka kwa Eric Shigongo James



Salaam ndugu yangu, Mara ya mwisho tulipoonana ilikuwa ni usiku pale Hospitali ya Aga-Khan ukiwa mgonjwa, tumaini langu ni kwamba unaendelea vizuri hasa kwa sababu ninakushuhudia mara kwa mara katika harakati unazoziendesha chini ya Ukawa. Nimeamua kukuandikia barua hii kwanza kabisa si kwa lengo la kukushambulia, siwezi kufanya hivyo hata siku moja. Nimewahi kukiri kwa mdomo wangu na maandishi kuwa miongoni mwa watu ninaowaheshimu sana katika nchi yangu ni James Mbatia, jambo hili kama hulijui basi naomba ulitambue tangu leo. Siwezi kukushambulia kwa sababu wewe ni raia mwenzangu wa Tanzania, siwezi kukushambulia kwa sababu siku zote nimeamini Mbatia ni mzalendo, mtu ambaye kila anapozungumza huwa naona mawazo yake na yangu kuhusu nchi hii ni kama yanafanana. Mara zote nimekusikia ukiongea vizuri juu ya taifa letu Tanzania bila kujali tofauti za kiitikadi, dini wala kabila. Ninachokifanya hapa leo ni kukumbushana, hivyo ndivyo tulivyoagizwa kwamba unapomwona mwenzako anapotea, mkumbushe, badala ya kumwacha aendelee kuelekea shimoni. Hivyo naomba univumilie sana, ili niongee yaliyomo moyoni mwangu, mwisho wa siku si lazima uyachukue au uyatilie maanani, unaruhusiwa kabisa kuyapuuza. Mwandishi na mzungumzaji maarufu duniani, Dk. Steve Maraboli aliwahi kusema maneno yafuatayo na ninaomba nimnukuu; Sisi sote hufanya makosa, sisi sote tunapambana na jambo fulani, sisi sote hupata majuto sababu ya mambo tuliyofanya zamani. Lakini pamoja na hayo hatutakiwi kuyaishi makosa yetu, kuyaishi mapambano yetu, kuyaishi majuto yetu, bali tuelewe tuko hapa leo, yaani hii ni leo tuna uwezo wa kuibadilisha leo na hatimaye kuibadilisha kesho! Maneno haya ya Maraboli ndugu yangu Mbatia yanathibitisha kabisa kwamba hakuna mwanadamu asiyekosea, ukishaitwa jina hilo tu (mwanadamu!) lazima huwa unafanya makosa, lazima huwa una majuto! Mimi hufanya makosa mengi ndugu yangu, mimi hujuta mara nyingi, ingawa nilishakataa kuishi katika makosa na kuishi katika majuto. Lengo langu kukuandikia barua hii leo ndugu yangu James ni kukukumbusha, si kukuhukumu, kwamba siku moja utakuja kuwa shahidi wa hiki ninachokisema; UMEIUA NCCR-MAGEUZI kwa kukubali kumezwa na Chadema bila wewe kufahamu, huu kwangu ni ukweli, turuhusu wakati uendelee kusonga mbele ipo siku mimi na wewe tutakutana na kuzungumza. Kwa kukubali kwako kuwaunganisha wanaNCCR-MAGEUZI na Ukawa, hakika umekichimbia chama chako kaburi bila kufahamu. Nia ilikuwa njema ya kuongeza nguvu ili muweze kuing’oa CCM, jambo moja ambalo hukulifahamu ni kwamba ulikuwa ukishughulika na mwanadamu ambaye mimi siku zote naamini ni ‘clever’, mtu huyu si mwingine  bali ni Freeman Mbowe. Ukitaka kuamini kwamba Mbowe ni ‘clever’ angalia alikoitoa Chadema na alikoifikisha bila kuwa na digrii hata moja kichwani mwake! Huyu ndiye mtu ambaye ndugu yangu James Mbatia ulikutana naye, wewe ukiwa ‘intelligent’ lakini ukawa si ‘clever’ na kulitumbukiza tone la NCCR-MAGEUZI kwenye pipa la Chadema, ndugu yangu hiki ni kifo cha NCCR, amini usiamini. Kwa mujibu wa kamusi yangu, kuna tofauti kati ya neno intelligent na clever. Intelligent ni mtu mwenye uwezo mkubwa wa kufikiri juu ya jambo na kupata jibu, sifa hii ndugu yangu James Mbatia unayo, hakuna ubishi, Watanzania wote wanajua lakini kwa mujibu wa kamusi yangu, clever ni mtu mwepesi wa kuelewa, kujifunza na kupata majibu kwa kasi, hata kama hatumii elimu ya darasani, huyu ndiye Mbowe ambaye mimi na wewe tunamfahamu. Ndugu yangu James, naomba usikasirike, nipe muda niongee na nikupatie taarifa za wanachama wako huku chini, wanalalamika chama chao kimeuzwa, mwenyekiti wa chama chao kaweka maslahi binafsi mbele kwa kujiunga na Ukawa sababu Ukawa wakishinda yeye atapata madaraka, hayo ndiyo yanayosemwa! Wanadai ukiliangalia bango la Ukawa lenye picha ya Edward Lowassa mtaani, hauoni kitu chochote cha kuonesha kwamba kuna NCCR-MAGEUZI katika Ukawa, maana rangi ni ya Chadema, alama ya vidole viwili ndiyo pekee inayoonekana kwenye bango hilo na Chadema ndiyo chama pekee kinachotajwa! Sasa swali wanalojiuliza, NCCR-MAGEUZI yao iko wapi? Bila shaka wamemezwa na Chadema. Matarajio yaliyopo sasa hivi ni kwamba Ukawa itashinda na kuchukua dola, siwezi kuongea sana kuhusu hilo maana chini ya umoja huo mnazo nguvu, lolote linaweza kutokea! Swali ninalojiuliza mimi na ambalo pia wewe unatakiwa kujiuliza ni kwamba, hivi ikitokea CCM ikashinda, itakuwaje kuhusu chama chako NCCR-MAGEUZI? Utaanza tena kujenga msingi kuanzia chini? Kama nilivyosema hapo juu, siandiki haya kukuhukumu bali kukukumbusha na kama kuna uwezekano uanze kuchukua hatua hivi sasa za kuhakikisha NCCR-MAGEUZI inakuwa hai ndani ya Ukawa, inaonekana ndani ya Ukawa, badala tu ya wewe kuonekana kwenye runinga ukijibu hoja au kuongea na waandishi wa habari. Mbatia una akili nyingi mno, hivyo ndivyo ilivyo familia yako yote, dada yako Ndelakijo Kessy Mbatia ni mkali wa hesabu na nilisoma hivi karibuni kwamba yeye ndiye Kaimu Katibu Mkuu wa NCCR-MAGEUZI kwa hivi sasa, inakuwaje hulioni hili jambo linalokijia chama chako? Hakika kwa mara ya kwanza umethibitisha kwamba kumbe mwanadamu anaweza kuwa ‘intelligent’ lakini  akawa si ‘clever’. Tatizo hili ndilo limefanya  wafanyabiashara wa kimataifa ambao ni clever, kuwasainisha viongozi wetu wa Kiafrika mikataba mibovu ingawa wana elimu kubwa lakini si ‘clever’. Ndugu yangu Mbatia, Nakusihi utafakari jambo hili kwa undani, nakuomba sana udai kuonekana (Visibility)  kwa chama chako katika Ukawa, tofauti  na hapo umemezwa na huo ndio utakuwa mwisho wa NCCR-MAGEUZI au utakuwa na kazi kubwa sana kukirejesha kwenye hali yake baada ya uchaguzi huu ikitokea mkashindwa. Naomba niishie hapa, nakutakia kila la kheri katika mapambano yako, Mungu akubariki wewe, familia yako na pia ibariki nchi yetu Tanzania, katika uamuzi wowote utakaoufanya hapo mbele, nakuomba uiweke amani ya nchi yetu katikati ya maamuzi yako, hiyo ndiyo sababu Mungu amekupeleka Ukawa, usikubali kabisa nchi hii iingie katika machafuko.
Wasalaam,
Eric Shigongo James

Chanzo: Gazeti la Uwazi Mizengwe

No comments:

Post a Comment