Na Neophitius Kyaruzi
MWENYEKITI wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe amesema anaungana na Dk. Wilbrod Slaa katika harakati za kusimamia maslahi ya taifa kwa kupinga ufisadi na kuwataka baadhi ya wanasiasa kuacha kumshambulia badala yake wajibu hoja kuhusu tuhuma zinazomkabili Edward Lowassa. Zitto alitoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam juzi, ikiwa imepita siku moja tu baada ya Dk. Slaa kujitokeza mbele ya vyombo vya habari kuwaeleza Watanzania kuwa ameamua kustaafu siasa baada ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) alichokuwa anakitumikia, kukiuka ajenda kuu ya kulinda maslahi ya taifa na badala yake kimekaribisha wale aliowaita mafisadi, jambo ambalo alilifananisha na kuhamishia choo chumbani. Katika taarifa yake, Zitto ambaye alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chadema kabla ya kutimuliwa kwa madai ya usaliti kisha kuhamia ACT, alisema licha ya kukwaruzana na Dk.Slaa alipokuwa Chadema, linapokuja suala la maslahi ya taifa, yupo tayari kuungana naye katika harakati za kupinga ufisadi na kwamba kamwe hatarudi nyuma katika msimamo huo kwani dhamira kuu ya chama chake ni uzalendo. Zitto alichukua nafasi hiyo kutoa mtazamo wake na uamuzi
atakaouchukua kuhakikisha msimamo wa Dk. Slaa wa kulinda maslahi ya taifa, unaheshimiwa na kuenziwa badala ya kutumia majukwaa ya siasa kumshambulia pasipo hoja za msingi.
“Slaa hayupo kwenye ‘ballot’ (karatasi ya kupigia kura). Naona watu wanahangaika na Slaa. Wengine tuliamua kukaa kimya kwani hekima inataka hivyo. Kwa kuwa watu wameamua kumtukana Dk. Slaa ni lazima tutoke kulinda haki yake,” alisema Zitto na kuongeza: “Tutatoka na tutaungana na Slaa kuwasema walio kwenye ‘ballot’. Slaa hayupo kwenye ballot. Mwacheni. Jadilini hoja zake siyo kumjadili yeye. “Eti hata watu wasio na rekodi yoyote ya kupambana na ufisadi nchi hii leo wanainua midomo yao kumsema Slaa. Mmeanza. Tutamsaidia Slaa, tutamaliza,” Zitto alisisitiza na kuongeza: “Sina mapenzi na Slaa. Alihusika kuniletea shida kubwa ya kisiasa nilipokuwa napigania misingi ndani ya Chadema. Hata hivyo naipenda zaidi Tanzania kuliko tofauti zangu na Slaa. Ni lazima aheshimiwe na alindwe,”alisema. Zitto amejitokeza kuzungumzia suala hilo kutokana na maneno yanayotolewa na baadhi ya watu kufuatia hotuba ya Dk. Slaa aliyoitoa akimtuhumu mgombea urais wa Chadema na Ukawa (Umoja wa Katiba ya Wananchi), Edward Lowassa kuwa fisadi asiyefaa kuchaguliwa kuwa rais.
Taarifa zilizolifikia gazeti
hili kutoka kwa vyanzo vyake, zinasema kuwa wanasiasa hao hivi sasa wana mkakati wa pamoja wa kuwasambaratisha mafisadi wanaojisafisha kwa ulaghai ili kuingia madarakani. Chanzo chetu kimeendelea kueleza kuwa hivi sasa wanajipanga kuibua tuhuma mpya zinazomkabili Lowassa na hatimaye kuzunguka nchi nzima kumwaga sumu ili wananchi wajue ukweli kuhusu wagombea wasio wazalendo kwa taifa lao.
“Dk. Slaa ameandaliwa ziara ya kuzunguka nchi nzima kwa kile kinachoelezwa kuwa ni kuwaaga wanachama wa Chadema lakini nyuma ya pazia, anakwenda kumwaga sumu kwa wananchi ili wasimchague Lowassa, yaani hizi siasa za mwaka huu zina mambo mengi kweli,” kilisema chanzo chetu. Wakati akiwa Chadema, Zitto alikuwa mwanasiasa machachari aliyekuwa akiongoza kampeni ya kupinga ufisadi bungeni kwa kuibua madudu mbalimbali yaliyokuwa yakifanywa na baadhi ya viongozi wa serikali, hasa wakati alipokuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali, kabla ya kupoteza nafasi hiyo baada ya kufukuzwa Chadema na kujiunga na ACT-Wazalendo. Hata hivyo, taarifa za uhakika zinasema mara baada ya kuzungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam mwanzoni mwa wiki hii, Dk. Slaa alikwea pipa kuelekea nchini Italia, hivyo jitihada za gazeti hili kupata msimamo wake juu ya hamasa mpya kutoka kwa Zitto zilikwama.
No comments:
Post a Comment