Polisi wafanya upelelezi kubaini ni wa chama gani.
Mgombea
Ubunge Jimbo la Ubungo kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk. Didas
Masaburi (pichani), amekanusha taarifa za kufadhili vijana wanaodaiwa
kuandamana wakipinga aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema) kuondoka ndani ya chama hicho.
Dk.
Masaburi alikanusha taarifa hizo jana wakati akizungumza na waandishi
wa habari jijini Dar es Salaam kuhusiana na uvumi uliozagaa kwenye
mitandao ya jamii kuwa vijana 10 wanaoshikiliwa na Jeshi la Polisi kwa
sababu ya kuandamana bila ya kibali wakimtaka Dk. Slaa asiondoke kwenye
chama hicho walitumwa na yeye.
“Tuhuma
hizo si za kweli, hata kama ninaunga mkono hoja zilizotolewa na Dk.
Slaa kuhusiana na tuhuma za ufisadi dhidi ya viongozi waliohamia Chadema
kutoka CCM, lakini siwezi kufadhili maandamano ya wanachama wa Chadema
ya kushinikiza kubakia kwa Dk. Slaa ndani ya chama hicho,” alisema.
Alisema
vijana aliowapokea katika ofisi ya CCM Jimbo la Ubungo zilizoko Manzese
juzi baada ya kurudisha kadi za vyama vyao kikiwamo cha Chadema
walifanya hivyo kwa mapenzi yao wakisema wamechoshwa na hadaa katika
vyama walivyotoka. Aidha, Dk. Masaburi aliwataka viongozi wa Chadema
kujibu hoja zilizotolewa na Dk. Slaa badala ya kutafuta mchawi baada ya
kuona amewaumbua na wanachama wao wanakihama chama hicho.
Wakati
huohuo, Jeshi la Polisi mkoa wa Kinondoni, jijini Dar es Salaam
limesema linaendelea na upelelezi ili kubaini vijana walioandamana juzi
eneo la Morocco, jijini humo iwapo ni wanachama wa Chadema au la.
Juzi
vijana takribani 100 wanaodaiwa kuwa wanachama wa Chadema waliandamana
katika eneo hilo wakishinikiza kurudi katika chama hicho kwa aliyekuwa
katibu mkuu wake, Dk. Willibrod Slaa, ambaye alitangaza kujitoa na
kujitenga na siasa, huku akimtuhumu mgombea urais wa chama hicho,
Edward Lowassa, masuala mbalimbali ua ufisadi.
Kamanda
wa Polisi wa kanda ya Kinondoni, Camilius Wambura kupita msaidizi wake,
jana aliliambia Nipashe kuwa bado wanawashikilia vijana 10 kati ya 100
ambao walitawanywa kwa mabomu ya machozi baada ya kukaidi amri ya jeshi
hilo ya kutakiwa kutawanyika, huku wakiendelea na upelelezi kubaini
wanatoka chama gani.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment