CUF: Taarifa kwa waandishi wa Habari juu ya Kujiuzulu Mwenyekiti Prof. Lipumba
CUF: Taarifa kwa waandishi wa Habari juu ya Kujiuzulu Mwenyekiti Prof. Lipumba
Leo tarehe 6 Agosti, 2015 Profesa Ibrahim Lipumba aliitisha mkutano na
waandishi wa habari katika Hoteli ya Peacock, mjini Dar es Salaam na
kutangaza kwamba amejizulu nafasi yake kama Mwenyekiti wa Taifa wa Chama
Cha Wananchi (CUF).
Sisi kama Chama tumezipokea taarifa hizo na tunayaheshimu maamuzi yake.
Ni haki yake ya kikatiba na haki ya kidemokrasia kufanya maamuzi
anayoyaona yana maslahi kwake.
Bila shaka, Profesa Ibrahim Lipumba amekifanyia kazi kubwa Chama chetu
katika miaka 16 ambayo alikuwa Mwenyekiti wetu, nafasi iliyomfanya awe
kiongozi wetu mkuu. Kwa nafasi yake hiyo, pia ametoa mchango mkubwa
katika ujenzi wa demokrasia katika nchi yetu. Tunaithamini kazi hiyo na
tutaendelea kumheshimu kwa utumishi wake mkubwa kwa Chama chetu na nchi
yetu. Tunamtakia kila la kheri katika mipango yake ya baadaye.
Chama Cha Wananchi (CUF) ni taasisi na kinaendeshwa kitaasisi. Ndiyo
maana maamuzi yake yote yamekuwa yakifanywa kitaasisi kwa mujibu wa
Katiba na Kanuni za Chama. Kwa msingi huo, pamoja na ukweli kwamba
kuondoka kwa Profesa Lipumba katika safu ya uongozi kutaacha pengo hasa
katika kipindi hichi ambacho tunaelekea kwenye Uchaguzi Mkuu,
tunawahakikishia wanachama na wapenzi wa CUF na wananchi wa Tanzania kwa
ujumla kwamba Chama hichi hakitayumba.
Katika historia yake, CUF imepita katika dhoruba na misukosuko mingi
lakini mara zote kimeonesha uwezo mkubwa wa kuhimili dhoruba na
misukosuko hiyo na kukabiliana na athari zake. Hatuna chembe ya wasiwasi
kwamba hata mtihani huu tutauvuka na tunaamini tutaibuka tukiwa Chama
imara zaidi.
Katibu Mkuu ameagiza kuitishwa kwa vikao vya dharura vya Kamati ya
Utendaji ya Taifa na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa siku ya Jumapili,
tarehe 9 Agosti, 2015 ili kujadili hatua hiyo na kufanya maamuzi juu ya
hatua muafaka zinazopaswa kuchukuliwa katika kipindi hiki hadi hapo
Chama kitakapomchagua mwanachama mwengine kujaza nafasi hiyo ya
Mwenyekiti.
Katika kipindi hiki, Chama kinawataka wanachama na wapenzi wake wote
kuwa watulivu na wavumilivu na kusubiri maelekezo ya vikao vya juu vya
kitaifa vya Chama.
Mwisho kabisa, tunawahakikishia wanachama wetu na Watanzania wote kwa
ujumla kwamba CUF itaendelea na shughuli zake kama Chama na pia kama
mshirika katika UKAWA ambayo CUF ilikuwa ni katika waasisi wake.
Tunawahakikishia wanachama wetu na Watanzania wote kwa ujumla kwamba CUF
itatumia nguvu, uwezo, juhudi na maarifa yake yote kuhakikisha kwamba
inaulinda UKAWA ambao unaonekana kuwa mwiba kwa CCM. Tunatambua kwamba
kuna njama na mbinu kubwa na nyingi zinazofanywa na watawala kutaka
kuuvuruga na kuuhujumu UKAWA wakidhani kwamba watapata manusura.
Tumesema na tunaendelea kusema CCM mwaka huu hawana manusura. Watanzania
wameamua kuwan’goa, na watan’goka Tanzania Bara na Zanzibar kupitia
sanduku la kura tarehe 25 Oktoba, 2015. Wimbi hili kubwa la mabadiliko
halizuiliki tena.
HAKI SAWA KWA WOTE
ISMAIL JUSSA
KAIMU MKURUGENZI WA HABARI, UENEZI NA MAWASILIANO NA UMMA
06 AGOSTI, 2015
No comments:
Post a Comment