December 2014 baada ya shindano la Miss Tanzania kukamilika
liliingia kwenye headlines baada ya Baraza la sanaa la Taifa kutangaza
kulifungia shindano hilo kwa miaka miwili baada ya kujiridhisha kwamba
limekiuka taratibu lakini leo August 17 2015 Miss Tanzania imeingia tena
kwenye headlines baada ya Basata kutoa msamaha.
Hii hapa chini ndio taarifa iliyotolewa na BASATA.
Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limelifungulia shindano la urembo
la Miss Tanzania baada ya mwandaaji wake Kampuni ya LINO International
Agency Limited kufuata taratibu, kuomba radhi na kuyafanyia kazi baadhi
ya mapungufu yaliyojitokeza na kutekeleza masharti aliyopewa.
Itakumbukwa kuwa mnano tarehe 22/12/2014 BASATA liliwaandikia barua
LINO International Agency Limited ya kulisimamisha shindano la Miss
Tanzania kwa miaka miwili (Mwaka 2015 na 2016) na kuwaagiza kujipanga
upya na kurekebisha kasoro ambazo zimekuwa zikijitokeza mara kwa mara.
Mapungufu yaliyobainishwa ni pamoja na; mosi, kutokufuata Sheria,
Kanuni na Taratibu za uendeshaji matukio ya Sanaa nchini, pili
kutokuwasilisha nyaraka mbalimbali za shindano lake hususan mikataba ya
washiriki. Tatu kutumia mawakala wasiosajiliwa na kupewa vibali vya
BASATA.
Miongoni mjwa mapungufu ambayo Kampuni ya LINO imeyafanyia kazi ni
kuanza mchakato wa usajili wa mawakala – BASATA na kufanyia marekebisho
kanuni na taratibu za uendeshaji wa Mashindano ya Urembo ya Miss
Tanzania. Aidha, LINO imewasilisha muundo wa kamati ya uendeshaji wa
shindano yenye muelekeo wa kuzingatia jinsia.
Katika kuboresha na kurudisha hadhi ya shindano la Miss Tanzania,
LINO International Agency Limited imepewa kibali cha muda kisichozidi
miezi minne (4) kwa ajili ya maandalizi ya awali ikiwemo kukamilisha
usajili wa mawakala katika ngazi zote husika.
BASATA linapenda kuwafahamisha wadau wote wa Sanaa hususan wale wa
shindano la urembo la Miss Tanzania kwamba Kampuni ya LINO imetekeleza
maagizo ya msingi iliyopewa kama masharti ya kufunguliwa. Na kwamba
baada ya kufanyia kazi changamoto zilizokuwa zimejitokeza BASATA
limeyafungulia mashindano ya Miss Tanzania kwa masharti ya kukamilisha
changamoto zilizobakia.
Ni matarajio ya BASATA kwamba kampuni ya LINO itazingatia taratibu
zote za uendeshaji wa matukio ya Sanaa nchini na kwamba haitarudia tena
makosa yatakayopelekea kuliweka shindano hili katika hali ya kushuka
hadhi na kuzua sintofahamu katika jamii.
Sanaa ni kazi, tuipende na kuithamini
Godfrey Mngereza
KATIBU MTENDAJI
No comments:
Post a Comment